Kwa mujibu wa Shirika la Habari la AhlulBayt (a.s) – ABNA – kundi la maafisa wa juu wa zamani wa kijeshi na kijasusi wa Israel wamelalamikia vikali kuendelea kwa vita huko Gaza, wakitaka mapigano yakomeshwe mara moja na kufikiwa makubaliano ya usitishaji vita kwa ajili ya kuwaokoa mateka. Wametahadharisha kuwa vita hivi vimesababisha "kushindwa kimkakati" kwa Israel, huku wakikosoa pia msaada usio na masharti kutoka Marekani kuwa chanzo cha kuendelea kwa mgogoro huu. Wamesema kuwa vita hivyo vimetishia utambulisho na nafasi ya kimataifa ya Israel.
Katika tamko lisilo la kawaida lililotolewa na kundi hili lenye zaidi ya watu 600 waliowahi kushika nyadhifa za kiusalama na kidiplomasia (ikiwa ni pamoja na makamanda wa jeshi, Mossad, Shin Bet, na polisi), wamemtaka Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, kusitisha mara moja operesheni ya kijeshi dhidi ya Gaza. Katika video iliyotangazwa Jumapili, walieleza kuwa vita hii haijaleta ushindi wowote, bali imeisukuma Israel kuelekea "kushindwa kwa kihistoria".
Tamir Pardo, aliyewahi kuwa mkuu wa Mossad, alisema wazi katika taarifa hiyo:
"Dunia inashuhudia janga ambalo sisi wenyewe tumeliumba. Tumeficha nyuma ya uongo tulioutengeneza sisi wenyewe, na sasa uongo huo unauzwa kwa raia wa Israel na ulimwengu."
Akaongeza kuwa vita hii ingeweza kumalizika kwa mafanikio ya kijeshi zaidi ya mwaka mmoja uliopita, lakini kwa sasa haijazalisha chochote isipokuwa hasara na uharibifu.
Amos Malka, aliyewahi kuwa mkuu wa idara ya ujasusi wa kijeshi, pia alitoa onyo kuwa:
"Tuko karibu na ukingo wa kushindwa. Malengo ya awali ya kijeshi yalitimia muda mrefu uliopita, lakini kwa sababu za kisiasa – si za kijeshi – mapigano yanaendelea, na hali hii inaiathiri vibaya Israel kisiasa na kiusalama."
Wengine waliotia saini tamko hilo ni pamoja na Ehud Barak, Waziri Mkuu wa zamani wa Israel, na Yoram Cohen, mkuu wa zamani wa Shin Bet. Wote wamesisitiza kuwa kuwepo kwa jeshi la Israel ndani ya Gaza hakuna faida yoyote ya kimkakati, bali kumesababisha ongezeko la vifo vya wanajeshi na kudhoofisha hadhi ya Israel kimataifa.
Maafisa hao pia wameikosoa vikali Marekani kwa kuendeleza msaada wake kwa Netanyahu, na wamemwandikia barua Donald Trump wakimtaka amtie shinikizo Netanyahu ili akubali usitishaji vita na afikie makubaliano ya kuwaachia huru mateka 50 wanaoshikiliwa na Hamas.
Katika barua hiyo walimwambia Trump:
"Uliweza kuanzisha usitishaji wa mapigano nchini Lebanon, sasa ni wakati wa kufanya hivyo pia kwa Gaza. Hamas siyo tena tishio la kimkakati kwa Israel, na sisi tuna uwezo wa kushughulikia vitisho vilivyosalia."
Pia, walionya kuhusu sera za "mrengo mkali wa kiitikadi" ndani ya serikali ya Netanyahu, wakiwataja kwa majina mawaziri kama Itamar Ben Gvir na Bezalel Smotrich, wakisema kuwa kundi hili dogo lenye misimamo mikali limeipeleka Israel kwenye njia isiyo na mantiki, ambayo haitasaidia kuwaokoa mateka bali itaongeza hatari ya kuipeleka Israel katika upweke wa kidiplomasia na kushindwa kimkakati.
Tamko hili limetolewa huku maandamano ya wananchi wa Israel yakiongezeka, wakidai kusitishwa kwa vita na kuachiliwa kwa mateka.
Video zilizotolewa na Hamas zikionesha hali mbaya ya kiafya ya mateka wawili wa Israel zimezua hasira kubwa nchini humo na kuongeza presha dhidi ya serikali ya Netanyahu.
Wachambuzi wa masuala ya kisiasa wanasema tamko hili linaonesha mgawanyiko mkubwa katika muundo wa kiusalama na kisiasa wa Israel. Wanaonya kuwa uungwaji mkono wa Marekani bila masharti kwa sera za kivita za Netanyahu umeifanya Israel kukwama kwenye mzozo wa kibinadamu wa muda mrefu huko Gaza, huku ikiingia katika hali ya kudhoofika isiyowahi kushuhudiwa na kujitenga na jamii ya kimataifa.
Your Comment